KARIBU SANA TOSA MAWE BLOG KWA HABARI MBALIMBALI TOKA PANDE ZOTE ZA DUNIA | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA PIA TUTUMIE HABARI MATUKIO KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI KWA SIMU: +447896103988 +447438590583 | E-mail: mwamfilingef@gmail.com NYOTE MNAKARIBISHWA SANA ASANTENI . | DO YOU NEED TO CREATE BLOG CONTACT US CLICK HERE | UNAHITAJI KUFUNGUA BLOG WASILIANA NASI BOFYA HAPA

Tuesday 16 June 2015

CCM INA WENYEWE,NA WATANZANIA NI WATU WAPOLE NA WASTAARABU SANA HAWANA MANENO KUHUSU UFISADI,HAWANA HABARI NA HOSPITAL NA SPIKA WAO ANAVYOONGEA BUNGENI,WABUNGE NAO KWA HIYO CCM INA WENYEWE TUSUBIRI



Kuna kisa cha msafiri mmoja aliyeomba mahali pa kulala kwa mjumbe wa Serikali ya Mtaa ili kesho yake aendelee na safari yake. Alifika saa 5.00 usiku na kwa kuwa mjumbe alikuwa amekwisha kula, alichofanya ni kumwandalia msafiri huyo mahali pa kulala, basi. 


Alishukuru. Mlo wake usiku ule ulikuwa machungwa sita aliyonunua njiani. Loo, alipokata la kwanza, lilikuwa limeoza, alitupa kwenye kona. Lahaula, alipochukua la pili, nalo lilikuwa limeoza. Balaa, kumbe yote yalikuwa vivyo hivyo.


Haraka aligundua kwamba kilichosababisha akaona machungwa kuwa yameoza ni kibatari, hivyo, alikizima, akachukua machungwa yale na kuanza kula gizani, akalala. Heri angelala na njaa kabisa maana kesho yake aliharisha sana njiani na kutapika; we acha tu!




Kisa hicho kinakaribia kujirudia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho makada wake waliotangaza nia au kuchukua fomu za kuwania urais wanachafuana na kujiozesha. Akisimama huyu anasema yeye tu anafaa, akisimama yule anadai wengine wote bomu, sasa atapatikana wapi aliye bora?


Edward Lowasa alijizuia alipotangaza nia, lakini Charles Makongoro alimshona barabara Stephen Wasira. “Mzee Wasira alifanya kazi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Nyerere aliondoka yeye akabaki, bado yupo. Akaja Ali Hassan Mwinyi akaondoka, yeye yupo….na sasa huyu Mzee Wetu Jakaya Kikwete anaondoka, atamuaga yeye atabaki yupo!” Hebu jiulize, ikitokea ‘Bwana Yupo’ ameteuliwa itakuwaje?


Frederick Sumaye hakutafuna maneno, alisema; “Kama kuna mtu mwingine amekamilika kuliko mimi niambieni, nitampisha (katika mbio za urais).” Alishangiliwa na wafuasi wake huku wakimwambia; “Hakunaaaa.”


Bernard Membe aliwaambia wanaCCM mkoani Lindi; “Nimetafakari sana, nimeona ninatosha kwa nafasi hii nyeti…, nafasi adhimu na si ya mzaha japo naona wapo wanaofanya mzaha. Nimeangalia nikaona hakuna mwingine wa kufanana na mimi.” Halafua akadai, “Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere huko aliko atafurahi endapo nitakuwa rais.” Yaani Nyerere afurahie Membe kuwa rais kuliko hata mtoto wake Makongoro?


Prof Sospeter Muhongo alisema; “Nafahamu... sidhani kama kuna mtu mwingine anafahamu kama mimi. Mkinipa ridhaa yenu wanaCCM, nitahakikisha tunatumia vyema fursa hizo kwa ajili ya manufaa ya uchumi wa Taifa hili….Mtu wa kufanya yote haya ndani ya CCM ni mimi, mnanijua vizuri…”


Samuel Sitta alijipigie debe kwa kusema; “Kwa kifupi ninao uelewa na uzoefu unaolingana na changamoto za kipindi kigumu cha miaka mitano ijayo yenye mwelekeo wa kutikisa misingi ya utawala wa nchi yetu… kwa uimara wangu wa uongozi, nitajumuisha nguvu na maarifa ya wananchi ili tuvuke salama na pia tutekeleze kazi za maendeleo kwa ufanisi na tija zaidi.”


Mwigulu Nchemba alisema; “Ahadi yangu kubwa kwenu ni kwamba nitawavusha. Nitawavusha wanaCCM wenzangu pamoja na Watanzania kwa ujumla… wakati ni sasa tunataka Taifa letu lifike kuwa nchi yenye uchumi wa kati.”


Kauli hizi zimetolewa kirejareja sana, lakini zitakuja kuwa na madhara makubwa mbele ya safari ndani na nje ya CCM kuwaaminisha wapigakura kwamba “chungwa teule” halijaoza kiviiile. Hapo watajitahidi kupiga msasa na kupinga methali isemayo “samaki mmoja akioza wote wameoza”.


Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa na mkutano mkuu wa CCM walioshiriki mwezi huu, kuwaunga mkono makada wanaowapenda wawe marais, ndiyo mwezi ujao, watashiriki kumpitisha mmoja akapambane na wa Ukawa kutafuta tiketi ya kuishi Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.


Nani akemee? Wazee wa kukemea walijazana Arusha, Butiama, Mwanza, Lindi, Mbeya na kwingineko kuwapiga ‘tafu’ watangazania.


Kingunge Ngombale-Mwiru, mmoja wa makada wenye hekima wanaotegemewa kutoa ushauri ndani ya CCM yuko katika Timu Lowasa. Siku Lowasa alipotangaza nia mjini Arusha, Kingunge alikuwapo na alitoboa siri ya Halmashauri Kuu akisema, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete aliwataka wale wenye ugomvi kutafuta suluhu. Vyema. Je, yeye kuwa kwenye Timu Lowasa ni kusaidia suluhu ipatikane?


Lowasa mwenyewe yuko tayari kwa suluhu? Akijibu maswali ya wahariri kuhusu kutofautiana na wenzake alisema; “…Kama kuna mtu ambaye hanipendi ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi.” Siku alipochukua fomu alisema, “Naamini katika ushindi na sina mpango wa kushindwa.” Waandishi wa habari walipomuuliza kama yupo tayari kushirikiana na wanasiasa wanaompinga sasa, aliwajibu; “Nitavuka daraja nitakapofika.” Mmh!


Ndiyo maana nasema zinakaribia siku za CCM kula gizani chungwa lililooza na kununua msasa ili kulitakatisha kabla ya kuliuza kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
KUPATA HABARI ZILIZOPITA BONYEZA OLDER POSTS