Baraza la usalama la umoja wa
mataifa limefanya kikao cha dharura kujadili madai kwamba wanajeshi wa
serikali ya Syria wametumia silaha za kemikali pale walipofanya
shambulio dhidi ya eneo lililopo nje kidogo ya mji mkuu wa Damascus hapo
jana jumatano.
Wanaharakati wa upinzani wamesema kuwa mamia ya
watu wakiwemo watoto wameuwawa huku muungano wa upinzani ukiyataja
mauaji hayo ya halaiki. Serikali ya Syria imekanusha kwamba imetumia
silaha hizo.
Mwenyekiti
wa baraza la usalama, Maria Parceval, ambaye ni balozi wa Argentinean
katika umoja wa mataifa amesema kuwa wanachama wa baraza hilo wameelezea
wasiwasi wao kuhusiana na madai hayo.
"Naweza kusema kuwa kuna wasiwasi mkubwa
miongoni mwa wanachama wa baraza kuhusu madai hayo. Kuna hisia kwamba
kuna haja ya kuwa wazi kuhusu kilichotokea na hali kufuatiliwa kwa
makini,'' anasema Bi. Maria Parceval.
''Wanachama wote wanakubaliana kwamba matumizi
yoyote ya silaha za kemikali, kwa yeyote katika mzozo huu, na katika
mazingira yoyote ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Kulikuwa pia na
makubaliano ya kutoa wito wa kusitishwa uhasama na vita.''
Kadhalika Bi. Perceval amesema kuwa kulikuwa na makubaliano kuhusu haja ya kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusiana na swala hilo.
''Wanachama wa baraza la usalama wametaka katibu
mkuu aingilie kati ili kuhakikisha kuwa uchunguzi wa haraka na wa kina
usioegemea upande wowote unafanywa. Wanachama wa baraza wameelezea haja
ya kutolewa mara moja msaada wa kibinadamu kwa waathiriwa. Hatimaye
baraza la usalama limetoa rambi rambi kwa waathiriwa pamoja na familia
zao,'' ameongeza kusema Bi. Maria Perceval, mwenyekiti wa baraza la
usalama la Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment