Chalinze. Mshindi wa kura za maoni za kugombea
ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya CCM, Ridhiwani Kikwete amesema
siasa anazofanya sasa hazina uhusiano wala ubia na baba yake.
Akizungumza
na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya
kura za maoni za chama hicho katika jimbo hilo kwenye Uwanja wa Shule ya
Msingi Msata alisema anafanya siasa kwa maisha yake na si kwa mgongo wa
baba yake kwani aliingia katika siasa akiwa na umri wa miaka mitano na
hakuwahi kufanya hivyo kwa sababu ya baba yake.
“Siasa
ninayofanya haina uhusiano na baba yangu, nafanya siasa kwa maisha yangu
na sina ubia na baba yangu katika hili” alisema mtoto huyo wa Rais
Jakaya Kikwete.
Akijibu swali la kwa nini amejiingiza
katika siasa tofauti na maneno yake aliyowahi kutamka mwaka 2010 kuwa
hawezi kushiriki katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo,
Ridhiwani alisema wakati huo hakuwa tayari.
“Kwenye
siasa usiwe muwazi katika kila kitu, ukiwa hivyo unawapa nafasi maadui
kukushambulia, mimi hapa Chalinze ni kwetu, kwa wazazi wangu na kule
Bagamoyo tunakwenda tu kikazi na ndiyo maana nikaamua kurudi nyumbani
kuomba ridhaa. Nashukuru kuongoza katika kura za maoni ninaona ni kiasi
gani ninaungwa mkono,” alisema.
Katika kura hizo za
maoni Ridhiwani alibuka mshindi kwa kura 758, akifuatiwa na Imani Madega
aliyepata kura 335, Ramadhan Maneno (206) na Mkwazu Changwa (17).
Kamati
Kuu ya CCM (CC), inatarajiwa kukutana Machi 8, mwaka huu kupitisha jina
mgombea wake wa ubunge katika jimbo hilo nafasi ambayo iliachwa wazi na
Said Bwanamdogo aliyefariki dunia Januari 22, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment